Licha ya kuwa na ushindani mkubwa wakati wa kampeni, CCM ina mizizi imara ambayo vyama vingine bado havijafanikiwa kuitikisa. Ushindani wa CCM na vyama vingine unajitokeza zaidi katika majukwaa ya kisiasa, lakini katika sanduku la kura, ushindani ni mdogo kwa kuwa CCM ina mtaji mkubwa wa wafuasi na wanachama ambao wanapojitokeza kupiga kura, ushindi wa CCM unakuwa rahisi, mbali na hoja za kisera na mitazamo ya vyama vingine.
IDADI YA WANACHAMA WA CCM
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Ndugu Steven Masira, ni kwamba CCM ina wanachama takriban milioni 12.5. Ikiwa kila mwanachama ataleta mtu mmoja, CCM itakuwa na kura takriban milioni 25. Hivyo, CCM bado ina uhakika wa kushinda katika kila uchaguzi wa kushika dola.
AZIMIO LA ARUSHA
Mnamo mwaka 1967, ilipitishwa Azimio la Arusha na Halimashauri Kuu ya TANU, lililofanyika Arusha. Azimio hili lilikuwa na lengo kuu la kupitisha falsafa ya kuondoa unyonge wa binadamu na kumkomboa mweusi kutokana na unyonyaji wa kibeberu, huku pia likilenga kuondoa matabaka katika jamii.
MISINGI YA AZIMIO LA ARUSHA (1967)
Misingi ya Azimio la Arusha ilikuwa ni:
- Usawa wa binadamu
- Utu wa binadamu
- Udugu
- Ujamaa na Kujitegemea (siasa ya ujamaa na kujitegemea)
- Uchumi wa dola (vyanzo vyote vya uchumi vilimilikiwe na serikali - uchumi wa kikanuni)
Misingi hii ilipitishwa na Halimashauri Kuu ya TANU, na baadaye, mwaka 1977, TANU na ASP zilipoungana na kuunda CCM, chama kililenga kudumisha misingi hii ya Azimio la Arusha.
JE, CCM INAISHI MISINGI YA AZIMIO LA ARUSHA?
Jibu ni rahisi: ndiyo, CCM bado inaamini na inaendelea kuishi kwa misingi ya Azimio la Arusha. Hii inajidhihirisha katika maeneo mbalimbali:
Utu wa binadamu: CCM imekuwa mstari wa mbele katika kutetea utu na heshima ya kila binadamu, bila kujali tofauti za kiideolojia. Mfano, kupitia kwa Katibu Mwenezi, CPA Makala, CCM iliendesha mchango wa kutengeneza gari la Ndugu Tundu Lissu, ambaye ni mkosoaji mkubwa wa serikali. Hili ni uthibitisho kwamba CCM inazingatia misingi ya Azimio la Arusha.
Usawa wa binadamu: CCM inaamini katika usawa wa binadamu. Mfano, katika sera ya elimu iliyoanzishwa hivi karibuni, elimu ya msingi hadi sekondari imetangazwa kuwa bure. Hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha usawa kwa watoto wote wa Tanzania, bila kujali hali ya kifamilia. Aidha, CCM inaendelea kuhakikisha usawa katika ajira na fursa zinazopatikana nchini.
Udugu wa binadamu: Viongozi wa CCM huita kila mmoja ndugu, na hii inaonyesha kwamba CCM ni familia moja yenye umoja na mshikamano. Huu ni mfano wa chama kikubwa cha siasa kilichojitahidi kuwa na ideolojia thabiti inayozungumzia umoja, udugu na usawa, jambo linalofanya CCM kuwa mfano wa vyama vikubwa barani Afrika na duniani.
Uchumi wa dola: Kwa kuwa CCM ni chama kinachoendelea na mabadiliko ya kiuchumi duniani, baadhi ya misingi ya Azimio la Arusha imeachia sekta binafsi kufanyakazi kwa sera ya ubinafsishaji. Hata hivyo, kuna misingi fulani inayozingatiwa, mfano, reli ni mali ya serikali na mashirika ya umma kama Shirika la Posta na Shirika la Umeme (TANESCO), vikiendelea kumilikiwa na serikali.
Falsafa ya siasa za ujamaa na kujitegemea: Ili kuondoa unyonge wa binadamu kama ilivyokusudiwa na Azimio la Arusha, ni muhimu kwa taifa kujitegemea. Mfano mzuri ni bajeti ya serikali ya mwaka 2024/2025, ambayo inategemea asilimia 70 ya mapato ya ndani. Hii ni ishara kwamba CCM bado inaishi kwa misingi ya Azimio la Arusha.
HITIMISHO
Ni ukweli usio pingika kuwa misingi ya Azimio la Arusha imewezesha taifa letu kuwa moja, kwani ililenga kuondoa utabaka, ukabila na tofauti za kijamii. Mfano mzuri ni sera ya utaifishaji wa shule na taasisi, ili kuhakikisha maslahi ya wananchi wote. Hivyo, sisi wananchi hatuna budi kuendelea kukiamini Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kuongoza dola na serikali.
Makala hii imeandikwa na:
John Francis Haule
Mkuu wa Soko Kuu la Arusha
0756717987 au 0711993907
John Francis Haule
0 Comments