Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU), mkoa wa Shinyanga, imeendesha warsha kwa wadau ambao ni wasimamizi wa miradi ya maendeleo na rasilimali za umma, ikilenga kuwajengea uwezo katika kuelekeza nguvu kwenye ufatiliaji wa miradi Mkoani humo.

Akizungumza katika uzinduzi wa warsha hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita amesema, serikali kwa kushirikiana na TAKUKURU mkoani Shinyanga, wamekuwa wakifanya jitihada katika kutoa elimu juu ya vitendo vya rushwa kwa watumishi wa umma, ili kuzuia vitendo hivyo.

“Ndugu zangu wakati mnaendelea kwenda kupambana, tayari fedha na ubadhirifu utakuwa umeshafanyika kwenye miradi ya maendeleo ambayo rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dr Samia Suluhu Hassan ametoa fedha hizo kwa ajili ya kutatua changamoto za wananchi, sasa tukingojea wakati hasara imeshatokea sawa tutashughulika na mhusika lakini wakati huo fedha zitakuwa zimepotea,” amesema RC Mhita.

Amesema, Serikali itaendelea kuwekeza katika kuwasaidia watumishi na kuhakikisha wanapata uelewa ili wasijiingize kwenye changamoto ya vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa fedha za umma katika miradi ya maendeleo pamoja na kuokoa fedha ambayo dhamira ya serikali ni kurahisha maisha ya wana Shinyanga.

Ameongeza kuwa, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo juu ya kupambana na rushwa ndio sababu hata TAKUKURU imewezeshwa kimfumo, miundombinu na kiuchumi, ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi katika kufatilia vitendo vya rushwa.

“Katika hili watu hawangaliani usoni anaweza akawa RC, DC, RAS au Mkurugenzi yeyote atakayehusika na matukio haya sheria ni msumeno utapita nae,” amesema RC Mhita.

Akielezea hali ya rushwa katika mkoa wa Shinyanga naibu mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Shinyanga Mwamba Masanja amesema utekelezaji wa vitendo vya kupambana na rushwa umekuwa ukifanyika kwa ufasaha kupitia madawati ya uchunguzi, uelimishaji umma, uzuiaji rushwa, pamoja na huduma za sheria na mashitaka.

Mwamba amesema majukumu hayo yamekuwa yakitekelezeka katika ngazi ya mkoa na katika wilaya ya za mkoa huo,na kuanisha kuwa kuwa TAKUKURU Shinyanga imekuwa ikiongeza jitihada Zaidi katika kuzuia vitendo vya rushwa huku nguvu kubwa ikielekezwa kwenye eneo la uelimishaji na ufatiliaji wa matumizi ya fedha za serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Akizungumzia program ya TAKUKURU rafiki Mwamba amesema taasisi hiyo imekuwa ikishirikana na wadau mbalimbali kuibua kero na kuzitolea majawabu na kuanisha kuwa kero hizo zisingetatuliwa zingepelekea uwepo wa vitendo vya rushwa na wakati mwingine kutokamilika kwa miradi ya maendeleo.

Nao baadhi ya wadau walioudhuria warsha hiyo wameipongeza TAKUKURU kwa kuwajengea uwezo katika kuona umuhimu wa ufatiliaji wa rasilimali za umma na kwamba watakwenda kutekeleza waliyofundishwa kwa vitendo ili kukabiliana na vitendo vya rushwa katika maeneo yao ya kazi.