Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeitaka Serikali kupitia Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kupanua wigo wa usimamizi wa masuala ya usalama na afya ili kuifikia sekta isiyo rasmi ambayo inakabiliwa na changamoto nyingi zaidi za usalama na afya mahali pa kazi.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Hawa Chakoma, wakati akihitimisha kikao baina ya Kamati hiyo na Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano) ambacho kilikuwa ni maalum kwa ajili ya kupokea taarifa kuhusu muundo na majukumu ya Taasisi za OSHA na WCF Bungeni Jijini Dodoma leo (Januari 19, 2025).
Mheshimiwa Chakoma ameipongeza Taasisi ya OSHA kwa kazi nzuri ya kuimarisha afya na usalama wa wafanyakazi nchini kupitia miongozo na ushauri unaotolewa na wataalam wa OSHA wanapotembelea na kufanya ukaguzi wa mifumo ya usalama na afya katika maeneo mbalimbali ya kazi nchini.
Amesisitiza umuhimu wa OSHA kuweka utaratibu wa kufuatilia utekelezaji wa maboresho ambayo yamekuwa yakitolewa kupitia kaguzi zao ili kuhakikisha kwamba
waajiri wanayafanyia kazi ipasavyo.
“Sisi kama Kamati licha ya kuwapongeza kwa kazi yao, tumewataka kuweka utaratibu endelevu wa kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara kwasababu kuna taarifa ya uwepo wa waajiri ambao wamekuwa wakizingatia matakwa ya Sheria ya Usalama na Afya Mhali pa kazi pindi wanapotembelewa na wakaguzi wa OSHA. Kinyume na hapo kunakuwa na upuuziaji wa kanuni na taratibu za kuwalinda wafanyakazi katika shughuli za uzalishaji,” ameeleza Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii.
Aidha, Kamati imeishauri serikali kuangalia namna bora ya kuijumuisha sekta isiyo rasmi katika mfumo rasmi wa usimamizi taratibu za usalama na afya ili kulinda nguvukazi kubwa iliyojiajiri katika sekta isiyo rasmi zikiwemo sekta ya usafirishaji na ujenzi.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati hiyo ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mwanza, Mhe. Kafiti William Kafiti amesema kupitia kikao hicho Kamati imepata fursa
ya kuelewa kwa undani namna ambavyo Taasisi hizo muhimu chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano) zinavyotekeleza majukumu yake ya msingi jambo ambalo litaleta tija katika utekelezaji wa jukumu la msingi la Kamati hiyo la kuishairi Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira na Mahusiano pamoja na Taasisi chini yake.
Akiwasilisha taarifa kuhusu muundo wa majukumu ya Taasisi za OSHA na WCF ambazo zipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Waziri mwenye dhamana ya Masuala ya Kazi, Mhe. Deus Sangu, ambaye aliambatana na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda na watendaji wengine wa Ofisi yake, ameieleza Kamati hiyo umuhimu wa majukumu ya Taasisi hizo mbili katika kuchochea maendeleo
na kuleta ustawi wa wafanyakazi na waajiri nchini.
OSHA ni miongoni mwa Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira na Mahusiano yenye jukumu la kusimamia utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Usalama na Afya Mahali
pa Kazi ya mwaka 2003 inayoweka msingi wa kitaifa wa usimamizi wa masuala ya usalama na afya katika shughuli zote za kiuchumi ili kulinda nguvukazi na uwekezaji nchini.




0 Comments