Wachimbaji madini katika Mgodi wa Mwabomba, Kata ya Idahina, Jimbo la Ushetu, wameeleza kuwa amani na utulivu ni nguzo muhimu katika shughuli za uchimbaji, wakisema bila hali hiyo kazi zao haziwezi kufanyika kwa ufanisi wala kuleta tija kwao na taifa kwa ujumla.Baadhi ya wachimbaji hao, akiwemo Juma Ngosha na Mabula Mayala, wamesema mazingira ya amani yamekuwa yakichochea ukuaji wa shughuli za uchimbaji, kuongeza uzalishaji na kuwavutia wawekezaji, huku wakibainisha kuwa migogoro au hali ya sintofahamu inaweza kuhatarisha usalama wao pamoja na uchumi wa eneo hilo.
Aidha, wachimbaji hao wameiomba serikali kuwapatia Soko la Dhahabu katika eneo la Mwabomba ili kuwawezesha kuuza madini yao kwa urahisi na kwa bei stahiki, badala ya kulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata masoko yaliyopo.
Wamesema uwepo wa soko hilo utasaidia kuongeza mapato yao na kudhibiti biashara holela ya madini.
Kwa upande wake, Serikali ya Halmashauri ya Ushetu imesema ipo katika maandalizi ya kuweka utaratibu wa kuanzisha Soko la Dhahabu Mwabomba, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha sekta ya madini na kuongeza mapato ya halmashauri pamoja na wananchi.
Naye Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Emmanuel Cherehani, ameahidi kulifanyia kazi suala hilo, akieleza kuwa atashirikiana na mamlaka husika kuhakikisha wachimbaji wanapata soko litakalowarahisishia shughuli zao na kuchochea maendeleo ya eneo hilo.
0 Comments