

Issa Mbaraka aliyekuwa mwenyekiti wa mpito wa stend united.
Na mwandishi wetu
Mwenyekiti wa mpito wa timu ya Stand United amejiuzulu nafasi yake kufuatia changamoto za kiuongozi ndani ya timu hiyo, hususan tofauti za kimtazamo katika uendeshaji.
Akizungumza na vyombo vya habari mkoani Shinyanga Mei 1, Ndugu Issa Mbaraka alithibitisha uamuzi wake huo, akieleza kuwa hatua hiyo imelenga kuinusuru timu ya Stand United.
Mbaraka alisema aliteuliwa na wadau kushika nafasi hiyo kuanzia Novemba 2025, kwa lengo la kusimamia na kurejesha timu katika ushindani mzuri wa soka.
Aidha, alibainisha kuwa sababu kuu ya kujiuzulu kwake ni kukosekana kwa ushirikiano kutoka kwa baadhi ya viongozi aliokuwa akifanya nao kazi.
“Nimetangaza rasmi leo kuwa sitahusika tena na usimamizi wa timu ya Stand United, kwa kuwa mtazamo wangu wa uongozi unatofautiana kabisa na viongozi wenzangu, hali inayoniwekea vikwazo katika utekelezaji wa majukumu yangu,” alisema Mbaraka.
Aliongeza kuwa alipoikuta timu ilikuwa haifanyi vizuri, lakini alijitahidi kuirejesha katika hali nzuri na kuanza kupata matokeo chanya. Hata hivyo, baadaye aligundua kuwepo kwa tofauti kubwa za kimtazamo miongoni mwa viongozi, jambo analobainisha uwepo wa vikwazo katika uendeshaji wa timu.
“Niliona ni vyema kuwaachilia waendelee na mfumo wao waliouzoea na usio na nia njema ya kuifikisha timu katika ustawi mzuri,nimeamua kulinda heshima yangu niliyojenga kwa jamii kwa muda mrefu,” amesema Mbaraka.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Shinyanga, Said Mankilingo, alisema kuwa amepokea taarifa hizo kupitia vyombo vya habari, na kumshauri Mbaraka kuwasilisha nakala rasmi barua ya kujiuzulu baada ya kuiandikia kamati tendaji ya timu ya stendi.
Aliongeza kuwa kama angepata fursa ya kuzungumza naye kabla ya uamuzi huo, angeweza kumshauri ipasavyo ili kupata suluhu ya changamoto zilizokuwepo.
0 Comments