6/recent/ticker-posts

MENEJA CHEKANI AWAITA WANANCHI AMBAO BADO AWAJAJIUNGA NA FAHARI AFYA (BIMA YA AFYA KWA WOTE) SHINYANGA, AELEZA WALIVYO SAJILI WANUFAIKA ZAIDI YA 36,000

Meneja wa NHIF Mkoa wa Shinyanga, Franklin Chekani, 
Chanzo Shinyanga One Media.
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Mkoa wa Shinyanga, umesajili wanufaika zaidi ya 36,000, katika mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, tangu kuanza kwa utekelezaji wa zoezi hilo kupitia awamu mbili tofauti.

Akizungumza na SHINYANGA ONE MEDIA, Meneja wa NHIF Mkoa wa Shinyanga, Franklin Chekani, amesema katika awamu ya kwanza iliyoanza Machi 2026, jumla ya wanufaika 30,000 walisajiliwa, ambao wanatoka Kaya zisizokuwa na uwezo kupitia mpango wa TASAF, waliolipiwa gharama za usajili na Serikali.

Amesema awamu ya pili ilianza baada ya kuzinduliwa na Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mheshimiwa Mboni Mhita mnamo tarehe 22, Oktoba, 2026, ikihusisha makundi yote ya wananchi, ambapo mpaka sasa wamesajili wanufaika 4,000 kutoka kaya zisizokuwa na uwezo na wanufaika  2,000 kutoka makundi mengine ya jamii.

Meneja wa NHIF Mkoa wa Shinyanga, Franklin Chekani

Chekani amesema NHIF mkoa wa Shinyanga, inaendelea na juhudi za kuhamasisha wananchi na kusajili wale ambao bado hawajajiunga na mpango huo, ikiwa na lengo la kufikisha wanufaika 976,356 ifikapo Novemba 1, 2027, huku lengo la kitaifa likiwa ni kusajili wanufaika milioni 28.

Akifafanua kuhusu vifurushi na vigezo vya kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote, amesema wananchi wanaweza kuchagua kifurushi kulingana na mahitaji yao na masharti yaliyowekwa.

Amekitaja kifurushi cha kwanza kuwa ni FAHARI AFYA, ambacho kinagharimu shilingi 150,000 kwa mwaka ,kwa kaya ya  watu sita, ambao ni mwanachama mchangiaji na wategemezi wake watano.

Amesema wategemezi wanaoruhusiwa katika kifurushi hicho ni mwenza wa ndoa, watoto wa kuzaa wenye umri usiozidi miaka 21, wazazi wa kumzaa mchangiaji, ndugu zake wa damu wasiozidi umri wa miaka 21, watoto wa kuasili, watoto wa kufikia pamoja na wakwe, ambao wote kwa pamoja watanufaika na huduma muhimu za afya zisizopungua 372.

Amevitaja vifurushi vingine kuwa ni cha WANAFUNZI, ambacho kinagharimu shilingi 50,400 kwa mwaka kwa mwanafunzi mmoja na kinawahusu wanafunzi wa kuanzia elimu ya awali hadi vyuo vikuu.

Pia amekitaja kifurushi kingine kuwa ni cha UMOJA AFYA, ambacho  kinawahusu waliounda kikundi cha kuanzia watu  10 na kuendelea bila kujali uhusiano wao, ingawa wanatakiwa kuwa wanaishi eneo moja.

 Kupitia kifurushi hicho, kila mwanakikundi anatakiwa kuchangia shilingi 60,000 kwa mwaka.

Amezitaja nyaraka ambazo Mwanachama mchangiaji anapaswa kuziwasilisha wakati wa usajili  kuwa ni pamoja na vitambulisho vya Taifa (NIDA) vya mwanachama na mwenza wake, cheti cha ndoa kinachotambulika kisheria, vyeti vya kuzaliwa vya watoto pamoja na nyaraka nyingine zinazothibitisha uhusiano wa wategemezi wengine.

Kwa upande wa watumishi wa umma ambao tayari wanachangia bima ya afya kupitia mishahara yao pamoja na wastaafu, Chekani amesema wataendelea kupata huduma za afya  kwa kufuata utaratibu wa kawaida, huku wanafamilia wengine ambao hawakidhi vigezo vya masharti ya bima wanayotumia, watalazimika kujiunga na mojawapo ya vifurushi vya Bima ya Afya kwa Wote kulingana na mahitaji yao.

Pamoja na vifurushi hivyo, bado NHIF inaendelea kutoa vifurushi vilivyokuwepo awali, vya Tarangire, Ngorongoro, Mikumi, Serengeti na Tanzanite Afya.

Post a Comment

0 Comments