6/recent/ticker-posts

DC MKUDE AZINDUA PROGRAMU JUMUISHI YA TAIFA YA MALEZI ,MAKUZI NA MAENDELEO YA AWALI YA WATOTO SHINYANGA


Amo Blog na Misalaba Shinyanga.

Programu jumuishi ya Taifa ya makuzi na malezi ya awali ya mtoto (PJT – MMMAM) imezinduliwa leo Jumatano Septemba 20,2023 Mkoani Shinyanga huku waratibu wakiagizwa kuandaa mpango kazi utakaogusa maeneo yote ya kimkakati.

Programu hiyo inatekelezwa katika Mikoa 26 ya Tanzania bara ambapo uzinduzi kwa ngazi ya Taifa ulifanyika Desemba 13,2021 ambapo ilizinduliwa na Waziri wa maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maaluma Dkt. Dorothy Gwajima kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizindua programu hiyo kwa niaba ya mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, mkuu wa Wilaya ya Kishapu Joseph Mkude amewaagiza waratibu wa PJT – MMMAM kufanyakazi kwa ubunifu na kuandaa mpango kazi unaogusa maeneo yote ya kimkakati ikiwemo kuzifikia sekta za umma na sekta binafsi.

DC Mkude amewaomba wadau na watu wote watakaoshiriki kwenye PJT – MMMAM kuhakikisha wanatoa kipaumbele na kuweka mipango ya utekelezaji wa maeneo hayo kuanzia ngazi ya familia na maeneo ya kazi.

“Nawaagiza waratibu kufanyakazi kama timu ya ushindi kwa kuandaa mpango kazi unaogusa maeneo yote ya kimkakati na kuzifikia sekta za umma na sekta binafsi lengo ni kuwapa fursa waajiri na watumishi wao ili kuhakikisha wanatoa fursa na kipaumbele katika malezi, makuzi na malezi ya awali ya mtoto wakati wawapo kazini na nyumbani”.amesema DC Mkude

Awali akizungumza afisa maendeleo ya jamii Mkoa wa Shinyanga Bwana Tedson Ngwale amesema utekelezaji wa programu jumuishi ya Taifa ya makuzi na malezi ya awali ya mtoto (PJT – MMMAM) umelenga maeneo makuu matano (5) ya kimkakati ambayo ni pamoja na upatikanaji wa Afya bora kwa mtoto, lishe bora kwa mtoto, malezi ya mwitikio, usalama na ulizi wa mtoto pamoja na fursa za ujifunzaji wa awali.

Kwa upande wake mwakilishi kutoka shirika la ICS Sabrina Majikata amesema PJT – MMMAM imelenga kuwaimarisha watoto kuanzia umri 0 hadi miaka nane (8) ambapo amesema ni jukumu la kila mtu kuwalinda watoto wa kike na watoto wa kiume ili waweze kukua na kufikia utimilifu wao.

Baadhi ya viongozi wa serikali na wadau akiwemo katibu wa kampeni ya kupinga ukatili inayoitwa Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Mkoa wa Shinyanga,  Bwana Daniel Kapaya amesema programu PJT – MMMAM itasaidia kupunguza ukatili unaoendelea katika jamii.

Programu jumuishi ya Taifa ya makuzi na malezi ya awali ya mtoto (PJT – MMMAM) imezinduliwa leo Jumatano Septemba 20,2023 Mkoani Shinyanga na kuhudhuriwa na viongozi wa serikali, taasisi binafsi pamoja na wadau mbalimbali.

 















































































































































Post a Comment

0 Comments