6/recent/ticker-posts

BENKI YA NMB KANDA YA MAGHARIBI YATOA MSAADA WA VIFAA TIBA VYA MILIONI 24 HOSPITALI YA DR.JAKAYA KIKWETE KISHAPU SHINYANGA

Meneja wa NMB Kanda ya Magharibi Seka Urio (katikati) akimkabidhi Vifaa Tiba ,Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe.Annamringi Macha (kushoto) 

Na Amojmedia Shinyanga.

Benki ya NMB Kanda ya Magharibi imetoa msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya Shilingi Milioni 24.6 katika kataka Hospitali ya Dr.Jakaya Kikwete Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga ikiwa ni sehemu ya ushiriki wa Benki hiyo katika maendeleo ya jamii  kwani ina wajibu wa kuhakikisha jamii inayowazunguka inafaidika kutokana na faida wanayoipata.

Akizungumza leo Jumatatu Juni 5,2024 wakati wa hafla ya makabidhiano ya vifaa tiba hivyo, Meneja wa NMB Kanda ya Magharibi Seka Urio amesema Benki ya NMB ni kinara katika kujali na kujihusisha na masuala mbalimbali ya jamii hapa nchini na kwamba changamoto za sekta ya afya Tanzania kwa benki ya NMB ni jambo la kipaumbele, na hii ni kutokana na ukweli kwamba afya ni mtaji wa maendeleo kwa taifa lolote hapa duniani.

"Tulipopata maombi haya ya kuchangia maendeleo ya afya katika Wilaya ya Kishapu , tulifarijika na kuamua mara moja kuja kushirikiana nanyi ili kuwa chachu ya maendeleo ya sekta hii muhimu kwa jamii yetu. Na hasa katika Wilaya ya Kishapu hususani katika hospitali ya Wilaya hii ambapo jumla ya msaada huu tuliotoa una thamani ya Tshs 24.6",ameeleza Urio.

"Benki ya NMB imekuwa ikipokea maombi mengi sana ya kuchangia katika miradi ya jamii, lakini benki imejikita zaidi katika maeneo ya elimu, afya, na misaada ya hali na mali katika nyakati ngumu kama za majanga. Benki NMB tumekuwa mstari wa mbele kuchangia huduma za kijamii kwa lengo la kurejesha sehemu ya faida yetu kwa jamii. Ni kwa zaidi ya miaka saba mfululizo tumekuwa tukitenga asilimia 1% ya faida yetu kama sehemu ya uwajibikaji kwa jamii inayotunzunguka",ameeleza Urio.

"Tunatambua juhudi za Serikali ya awamu ya sita chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kusimamia upatikanaji wa huduma bora za afya kwa nguvu zote kwa kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma hizi mjini na vijijini; hatuna budi kuipongeza Serikali kwa hilo. Pamoja na makubwa mengi yanayofanywa na Serikali, sisi kama wadau tunao wajibu wa kuunga mkono juhudi hizi za maendeleo kwa kusaidia jamii zetu kwani jamii hizi ndio zimeifanya benki ya NMB kuwa hapa ilipo na kubwa kuliko benki yoyote hapa nchini. Tunatambua kuwa ni kupitia jamii ndipo wateja wetu wengi wanapotoka, kwa hiyo kurudisha sehemu ya faida kwa jamii ni utamaduni wetu",ameongeza Urio.

Aidha amebainisha kuwa, kwa miaka kadhaa sasa, NMB imekuwa ikisaidia miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi kwa kujikita zaidi kwenye miradi ya elimu (madawati na vifaa vya kuezeka), afya (vitanda, magodoro yake na vifaa vingine vya kusaidia matibabu) na kusaidia majanga yanayoipata nchi ya Tanzania.

Urio amefafanua kuwa Benki NMB ndiyo benki inayoongoza nchini huku tukiwa na matawi 230,na tunaendelea kuboresha huduma za kibenki kwa njia ya mitandao ili kuwafikia wateja wengi zaidi kwa njia rahisi na salama.

Akipokea vifaa tiba hivyo Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mhe.Annamringi Macha ameishukuru Benki ya NMB kwa msaada huo katika sekta ya afya huku akiwataka wahudumu wa afya kuvitunza vifaa hivyo ili viwe na manufaa na kuleta tija iliyokusudiwa.

Pia Mhe.Macha amewataka wananchi wa mkoa wa Shinyanga kujiunga na huduma za NMB Ili waondokane na mikopo umiza kwa kuwa benki ya NMB Inayo mikopo wa bei na fuutofauti na Taasisi nyingine zinazo jihusisha na utoaji wa mikopo.

Nao Diwani wa kata ya Kishapu Joel Son ameishukuru Benki ya NMB kwa kuendelea kuikumbuka sekta ya afya katika wilaya ya ya Kishapu.
Meneja wa NMB Kanda ya Magharibi Seka Urio (katikati) akimkabidhi Vifaa Tiba ,Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe.Annamringi Macha (kushoto) 
Meneja wa NMB Kanda ya Magharibi Seka Urio akizungumza wa kati wa kukabidhi vifaa tiba.
Wauguzi na watumishi wa benki ya NMB wakishiriki hafla ya kukabidhi vifaa tiba.
Watumishi wa Hospitali ya Dr.Jakaya Kikwete wakishiriki hafla ya kukabidhi vifaa tiba.

Tazama picha za matukio Chini.










Post a Comment

0 Comments