6/recent/ticker-posts

ENG.JUMBE ALIPA MILIONI 1.5 KUUJAZA UWANJA WA CCM KAMBARAGE “TWEN'ZETU KWA YESU 2025”


Mhandisi James Jumbe ameonesha tena moyo wa ukarimu na kujali maendeleo ya vijana kwa kutoa shilingi milioni 1.5, fedha alizotumia kununua tiketi 300 kwa ajili ya kuwawezesha vijana na washiriki wa tamasha kubwa la Twen'zetu kwa Yesu 2025, linaloandaliwa na Kanisa la KKKT Ebenezer kwa kushirikiana na Jambo FM.

Tamasha hilo, litakalofanyika Jumamosi, Agosti 16, 2025 katika Uwanja wa CCM Kambarage, mjini Shinyanga kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni, linabeba kauli mbiu ya “Ishi kwa Malengo” na linatarajiwa kuwa jukwaa maalum la uimbaji wa nyimbo za Injili, michezo, na mahubiri yenye mguso wa kiroho, likiwa na lengo la kuwajenga vijana kiimani, kiakili na kijamii.


Kwa kununua tiketi hizo na kuzigawa bure, Mhandisi Jumbe amepongezwa na waandaaji wa tamasha na wakazi wa Shinyanga kwa kuonyesha mfano wa kuigwa katika kuunga mkono shughuli za kijamii na kidini. Vijana waliofaidika wamesema msaada huo umeongeza hamasa ya kuhudhuria kwa wingi na kushiriki kikamilifu.

Mratibu wa tamasha hilo, Mchungaji Odolous Gyunda, amesema mgeni rasmi atakuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mheshimiwa Mboni Mhita, huku mnenaji mkuu akiwa ni Mhashamu Askofu Jackson Sosthenes wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam.

Tamasha litapambwa na burudani mbalimbali ikiwemo AGAPE Gospel Band na Neema Gospel Choir kutoka Dar es Salaam, Boaz Danken kutoka Mwanza, AICT Kambarage Choir, Malaika Wakuu wa Kanisa Katoliki Ngokolo, pamoja na kwaya za vijana kutoka KKKT DKMZV, Kwaya ya Sungusungu na wanamichezo wa mbio za baiskeli.

Post a Comment

0 Comments