6/recent/ticker-posts

WAFANYABIASHARA SHINYANGA WAIPONGEZA TRA KWA MABADILIKO YA SHERIA YA KODI 2025

Baadhi ya wafanyabiashara katika mkoa wa Shinyanga wameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kufanya marekebisho ya Sheria ya Kodi ya mwaka 2025, ikiwemo hatua ya kufuta kodi kwa baadhi ya watoa huduma ndogo za kijamii kama waendesha bodaboda na mama lishe.

Zenaida Rweisunga, mfanyabiashara wa Shinyanga, amesema marekebisho hayo ni faraja kubwa kwa wananchi na yatapunguza mzigo wa kodi kwa watoa huduma wadogo, huku akishauri TRA kuendelea kusikiliza maoni ya wananchi hususan kwenye suala la kodi ya nyumba.

Naye Fadhili Machum, mwendesha bodaboda mjini Shinyanga, ameishukuru TRA kwa hatua ya kufuta kodi kwa waendesha bodaboda akisema itawapunguzia gharama na kuwapa nafasi ya kuboresha maisha yao.

Mabadiliko hayo yameelezwa kwa kina na Afisa Mkuu Msimamizi wa Kodi wa TRA, Hamad Mterry, wakati akitoa elimu kwa wafanyabiashara na wananchi wa Shinyanga kuhusu sheria mpya za kodi zilizopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Marekebisho haya yamelenga kurahisisha ulipaji kodi na kupunguza mzigo kwa watoa huduma wadogo ili kuongeza wigo wa walipa kodi kwa hiari,” alisema Mterry.

Kwa upande wake, Jackton Koy, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wafanyabiashara Mkoa wa Shinyanga, ameipongeza TRA kwa kushirikiana nao kupitia elimu ya kodi, huku akiwasihi wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari kwa maendeleo ya taifa.

“Ni muhimu TRA waendelee kutukaribisha karibu na kuwasikiliza wafanyabiashara. Kwa upande wetu, ni wajibu wetu kulipa kodi kwa hiari kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu,” alisema Koy.

Elimu hiyo imeonekana kuongeza uelewa kwa wafanyabiashara wa Shinyanga juu ya wajibu wao wa kulipa kodi, huku wengi wakiahidi kuendelea kushirikiana na mamlaka hiyo kwa manufaa ya taifa.

Post a Comment

0 Comments