6/recent/ticker-posts

TAIFA GAS HAITAONGEZA BEI YA GESI

 


Meneja Mkuu wa Taifa Gas nchini Devis Deogratius
Taifa Gas haitapandisha bei ya gesi ya majumbani (LPG) licha ya ongezeko la takribani asilimia 43 ya bei ya gesi hiyo duniani. Hatua hii ni sehemu ya juhudi za kampuni hiyo kuendeleza upatikanaji nafuu wa nishati hiyo pamoja na kupunguza za athari za mabadiliko ya soko la kimataifa kwa wateja wake.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari Aprili 3, 2026, Taifa Gas imeeleza kuwa soko la kimataifa la gesi ya kupikia limekumbwa na ongezeko kubwa la bei katika wiki za hivi karibuni na hivyo kusababisha kuongezeka kwa gharama za ununuzi katika minyororo ya ugavi na usambazaji duniani.

“Katika mazingira haya ya sasa, tunayo dhamira ya dhati ya kuwasaidia wateja wetu kwa kubeba athari za ongezeko la gharama ya nishati ya kupikia kwa kutokuongeza bei huku tukihakikisha upatikanaji endelevu wa gesi safi na ya kuaminika,” alisema Meneja Mkuu wa Taifa Gas, Devis Deogratius.

Nishati Nafuu na Utulivu wa Kiuchumi

Taifa Gas imesema kuwa kipaumbele chake kwa sasa ni kuhakikisha bei hiyo ya nishati haiongezeki hivyo, kutoa mchango muhimu kwenye shughuli za kiuchumi huku ikitambua kuwa gesi ya kupikia ni nishati muhimu katika kaya na biashara ndogo ndogo nchini Tanzania.

Deogratius alisema, “Tunatambua kuwa gesi ya kupikia ni nishati muhimu kwa Watanzania wengi na lengo letu ni kuhakikisha kwamba inapatikana kwa bei nafuu huku tukidumisha usambazaji wa uhakika kote nchini.”

Upatikanaji na Usambazaji wa Gesi Nchini

Taifa Gas inauthibitishia umma kwamba usambazaji wa bidhaa zake utaendelea kuwa thabiti kupitia mtandao wake wa maghala 25 yaliyopo nchini kote hivyo, kuhakikisha upatikanaji wa gesi ya kupikia katika maeneo ya mijini na vijijini.

“Tanzania ni nchi kubwa na yenye mahitaji tofauti hivyo upatikanaji wa nishati hii ni kipaumbele kikubwa kwetu sisi,” alisema Deogratius na kuongeza kwamba, “Tumewekeza katika miundombinu inayotuwezesha kusambaza gesi ya kupikia sehemu mbalimbali nchini.”

Nishati Safi na Vipaumbele vya Kitaifa

Taifa Gas imeeleza kuwa inaendelea kuzingatia vipaumbele vya kitaifa vya nishati pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hasa katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na hivyo, kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.

Kampuni hiyo imeeleza kwamba upatikanaji wa LPG unachangia kuboresha afya za wananchi, kulinda mazingira, na kuchangia katika ushirikishwaji wa wananchi kwenye Uchumi wa nchi.

Dhamira Endelevu

Taifa Gas imesisitiza kuwa itaendelea kuufuatilia mwenendo wa soko la kimataifa huku ikiendelea kufanya kazi ndani ya mifumo ya sekta ya nishati ili kuwasaidia wateja kwa kudumisha utulivu wa bei kadri itakavyowezekana.

“Jukumu letu ni kuwauunga mkono na kuwalinda Watanzania kwa kuwapa huduma bora, kuwa na uendeshaji wenye uwajibikaji, na dhamira ya muda mrefu ya kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi nchini,” alisema Deogratius.


Taifa Gas ni kampuni ya nishati ya Tanzania inayojihusisha na usambazaji wa gesi ya majumbani (LPG.) Kampuni hii inaendesha kituo kikubwa zaidi cha kuhifadhi LPG nchini na ina mtandao mpana zaidi wa usambazaji wenye maghala 25 nchini kote. Kampuni hii imejikita katika kupanua upatikanaji wa nishati safi, nafuu na ya kuaminika.

Post a Comment

0 Comments