Mwenyekiti wa Tume ya Madini nchini, Bi Janet Lekashingo akizungumza na wafanyakazi na mameneja wa Mgodi wa Bulyanhulu wakati wa semina ya mafunzo ya siku moja kuhusu utekelezaji wa maudhui ya ndani (Local Content) na Uwajibikaji wa Jamii wajibu (CSR) iliyofanyika katika mgodi wa Bulyanhulu
Meneja Mkuu wa Barrick Bulyanhulu, Bw Victor Lule akieleza jambo wakati wa semina hiyo.
Ujumbe kutoka Tume ya Madini wakionyeshwa vifaa vya teknolojia ya kiditali ya uchimbaji mgodi wa Barrick Bulyanhulu
Ujumbe kutoka Tume ya Madini wakionyeshwa vifaa vya teknolojia ya kiditali ya uchimbaji mgodi wa Barrick Bulyanhulu
***
Tume ya Madini imeipongeza Migodi ya Barrick ambayo inaiendesha kwa ubia na Serikali kupitia kampuni ya Twiga kwa kutekeleza vyema sera ya maudhui ya ndani (Local content) na kuwawezesha Watanzania kushiriki katika kufanya biashara na makampuni ya uchimbaji madini, uwekezaji kwenye sekta husika na kuboresha ustawi wa jamii na uchumi kwenye maeneo yanayozunguka migodi hapa nchini.
Akizungumza katika semina ya mafunzo ya siku moja kuhusu utekelezaji wa maudhui ya ndani (Local Content) na uwajibikaji kwa Jamii (CSR) katika mgodi wa dhahabu wa Barrick Bulyanhulu, Mwenyekiti wa Tume ya Madini nchini, Bi Janet Lekashingo, amesema kuwa lengo la Serikali kuanzisha kanuni za muadhui ya ndani (Local Content) na Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) ni jitihada za kuhimiza uendelevu, ushirikishwaji na kutoa sehemu ya faida kwa jamii inayozunguka migodi husika.
“Hii sio tu kutimiza majukumu, bali ni kuunda mustakabali ambapo uchimbaji madini utakuwa na matokeo chanya na endelevu. Tangu kuanzishwa kwake, Tume ya Madini imekuwa mstari wa mbele na imara katika kuhakikisha kwamba bidhaa na huduma za watanzania zinapewa kipaumbele katika sekta hii,” amesema.
Amesema kwamba kwa kuweka kipaumbele kwenye maudhui ya ndani (Local Content) Tume hiyo imeona ongezeko kubwa la watanzania wanaonufaika moja kwa moja kutoka kwenye sekta ya madini ni ishara wazi ya maendeleo ukilinganisha na miaka iliyopita.
Amesema utekelezaji wa maudhui ya ndani ni kuhusu kuiwezesha jamii – kutengeneza ajira, kukuza biashara za ndani na kuboresha maisha ya watu wanaozunguka maeneo ya uchimbaji madini kwa kuwashirikisha moja kwa moja na njia isiyo ya moja kwa moja katika shughuli za biashara na uchimbaji madini.
“Tunapoanza semina hii, tukumbuke umuhimu wa maudhui ya ndani (Local Content) katika kufungua uwezo wa Tanzania. Hizi kanuni ni daraja linalowaunganisha watanzania kupata ujuzi wa kimataifa na za ndani, kuhakikisha kwamba sekta ya madini inakuwa nguzo ya maendeleo endelevu ya kitaifa,” ameeleza.
Alisema alifurahi sana kuona kuwa Mgodi huo Bulyanhulu na migodi mingine ya Barrick mameneja wake wote ni watanzania na aliwashauri makampuni mengine ya uchimbaji madini kuzingatia utekelezaji wa maudhui ya ndani.
“Ni muhimu kwa kampuni kuwawezesha wazabuni wa ndani kama sehemu ya jitihada za serikali na makampuni ya madini kujenga uwezo, kuunda na kukuza uelewa wa pamoja na ushirikiano”,amesema.
Bi. Lekashingo, ameshauri Migodi ya Barrick na Twiga kulenga miradi endelevu inayochangia ukuaji wa uchumi badala ya kuendelea kuagiza vipuri kutoka nje ni muhimu kuanza jitihada za kuanzisha viwanda vya vipuri hapa nchini.
Amesisitiza kuwa serikali iko makini kuona kuanzishwa kwa viwanda vinavyohudumia sekta ya madini kwa vile tayari eneo maalum la uchumi na uwekezaji limeshatengwa la Buzwagi kwa ajili ya wawekezaji wa ndani na nje kuja kuwekeza kwenye eneo hilo maalum kwa ajii ya kujenga viwanda.
Amesema pia wanapaswa kutafuta njia mbadala za kuanzisha viwanda vya vipuri ambavyo vitatoa ajira kwa watanzania na tutaweza kuuza nje ya nchini hivyo vipuri kwenye nchini zenye shughuli za uchimbaji wa madini kama vile DRC Congo.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Mgodi wa Bulyanhulu, Bw. Victor Lule, amesema kampuni hiyo alishukuru Serikali kwa kuanzisha sera hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa imeanza kupata mafanikio kwa kuwanufaisha Watanzania wengi.
“Kwa sasa, tuko kwenye njia sahihi kwani takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 82 ya manunuzi yetu ilifanywa na wasambazaji wa ndani, wakati asilimia 12 iliyobaki ilifanywa na wasambazaji wa kigeni. Tunaendelea kutekeleza kile tunachosema kuhusu utekelezaji wa maudhui ya ndani.”
Amesisitiza kuwa kampuni ya uchimbaji madini itaendelea kuwaelimisha wafanyabiashara na wasambazaji wa ndani jinsi ya kufanya biashara na makampuni ya madini jinsi ya kusajili kampuni zao na kushiriki katika semina, warsha na mikutano ili kujenga uelewa na uhusiano wa pamoja na endelevu.
Bwana Lule ameeleza kuwa kampuni hiyo Barrick Twiga asilimia 96 ya wafanyakazi wake ni watanzania, baadhi yao wakiwa katika ngazi ya uongozi, jambo ambalo ni Ushahidi tosha kwamba mgodi huo inakuza falsafa ya maudhui ya ndani. (local Content)
Ameongeza kuwa ni muhimu kwa wazabuni wa ndani kuwa waaminifu, wachapakazi na kutekeleza kazi na kukabidhi ndani ya muda wa makubaliano . aliongeza baadhi ya wasambazaji wa ndani walishindwa kutimiza majukumu yao na wakati mwingine walileta bidhaa chini ya viwango.
Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Madini na Biashara kutokaTume ya Madini, Bw Venance Kasiki, ameipongeza Barrick na Twiga kwa utekelezaji wa maudhui ya ndani kwa ufanisi, lakini pia akishauri kuzingatia kusaidia na kuwekeza kwenye miradi mikubwa na endelevu inayohusisha jamii.
Ameongeza kusema kuwa Tume ya Madini imekuwa na mikutano kadhaa na taasisi za kifedha nchini benki za ndani kuanza kuwawezesha wazabuni wa ndani katika sekta ya madini kama vile kutoa mikopo kama hatua za awali za kurahisisha utekelezaji wa maudhui ya ndani.
“Tuna mikutano kadhaa na majadiliano na benki mbalimbali nchini kama vile CRDB, NMB na nyingine ili kuanza kuangalia sekta ya madini kama sekta inayokua kwa kasi na yenye matokeo Chanya na si hatari tena,” amesema.
0 Comments