
#Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Aeleza Mafao na Faida za Skimu ya Hifadhi
Na MWANDISHI WETU,
Mwanza.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, ameongoza utoaji wa elimu ya hifadhi ya jamii kwa wananchi waliojiajiri Kanda ya Ziwa, huku akiwahamasisha kujiwekea akiba kwa ajili ya maisha yao ya sasa na baadaye.
Alisema hayo wakati wa muendelezo wa utoaji wa elimu ya Skimu ya Hifadhi uliofanyika katika Soko la Kimataifa la Samaki Kirumba jijini Mwanza, tarehe 6 Machi 2026.
Katika ziara hiyo ya kikazi, Waziri Sangu aliangalia shughuli za wajasiriamali wakiwemo wavuvi na kushiriki kuvua samaki pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba.
Ziara hiyo imemsaidia kuelewa mazingira ya kazi ya wananchi wanaolengwa na skimu hiyo.
Aliwataka wananchi wa Mwanza na mikoa jirani kujiunga na NSSF ili kujiwekea akiba na kunufaika na mafao yanayotolewa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Waziri Sangu alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha wajasiriamali wanakuwa sehemu ya hifadhi ya jamii na kueleza kuwa skimu hiyo itasaidia Watanzania kuondokana na umaskini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, alisema mkoa umejipanga kuandikisha wanachama wengi zaidi iwapo hamasa kubwa itaendelea.
“Sekta ya waliojiajiri imeimarika sana; wananchi wengi wanajihusisha na uvuvi, kilimo na shughuli nyingine za kipato. Kwa hamasa kama hii, tutawaandikisha wengi zaidi na kunufaika na mafao yanayotolewa na NSSF,” alisema.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba aliwataka waliojiajiri kujiunga na kuchangia skimu hiyo, ambapo wananufaika na mafao mbalimbali ikiwemo pensheni ya uzee, urithi, ulemavu, matibabu na huduma nyingine.
Alibainisha kuwa mfumo wa uchangiaji ni rafiki, ukiwa na kiwango cha chini cha shilingi 30,000 au 52,200 kwa mwezi, kinachowawezesha wanachama na familia zao kunufaika.
Awali, Mbunge wa Ilemela, Mhe. Kafiti Kafiti, aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwajumuisha wananchi waliojiajiri kunufaika na hifadhi ya jamii kama wanavyonufaika wafanyakazi wa sekta binafsi na sekta ya umma.
“Ndugu zangu, kupata pensheni sio lazima uwe mtumishi wa Serikali au sekta binafsi. Yeyote anayejipatia kipato sasa ana fursa hiyo.
Milango imefunguliwa, na mimi kama balozi wa bodaboda na bajaji tunaendelea kufungua fursa ili watu wajiajiri, wachangie na kujiwekea akiba ya baadaye kupitia Mfuko wa NSSF,” alisema Mhe. Kafiti.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu akijionea shughuli za uvuvi katika maeneo ya kazi ya wavuvi katika Soko la Kimataifa la Samaki Kirumba jijini Mwanza, ambapo pia alishiriki kuvua samaki akishirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba.

.jpeg)










0 Comments