6/recent/ticker-posts

WAZIRI KAPINGA ; MCHANGO WA SIDO KATIKA UKUAJI WA UCHUMI NA KUZALISHA AJIRA NCHINI NI MKUBWA

Na George Mganga, Kahama MC

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, amesema Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) limeendelea kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi wa viwanda nchini kupitia uwezeshaji wa wajasiriamali, akieleza kuwa ndani ya kipindi cha miaka mitatu shirika hilo limefanikiwa kuanzisha viwanda 1,760 na kuzalisha zaidi ya ajira 60,000.

Amesema mafanikio hayo yanaonesha umuhimu wa kuwekeza katika wajasiriamali wa ndani ili kuongeza uzalishaji, kupanua fursa za ajira na kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa nchini, hatua inayoweza kuongeza kipato cha wananchi na kuimarisha uchumi wa Taifa.

Mhe. Kapinga ameyasema hayo Oktoba 24, 2026, wakati akizindua rasmi Maonesho ya 5 ya SIDO Kitaifa katika Uwanja wa Magufuli, Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga, yaliyowakutanisha wajasiriamali na wadau mbalimbali wa sekta ya umma na binafsi.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, baada ya kuwasili katika uwanja wa Magufuli mjini Kahama

“Tunapoangazia kujenga uchumi wa Taifa, tunaweka nguvu katika uwekezaji wa ndani ili kuongeza uzalishaji na kukuza uchumi. Hilo ndilo mojawapo ya malengo ya kuanzishwa kwa SIDO,” amesema Mhe. Kapinga.

Amesisitiza kuwa Serikali inatarajia kuona wajasiriamali wakitoka katika hatua ya kuuza mazao ghafi na kuelekea katika kuyachakata kwa kutumia teknolojia zinazofaa, ili kuongeza thamani ya bidhaa, kupanua masoko na kuongeza mapato yao.

Amesema uwekezaji katika teknolojia za uchakataji ni muhimu kwa kuwa utawasaidia wananchi kutumia rasilimali zinazopatikana katika maeneo yao kuzalisha bidhaa zenye thamani kubwa zaidi, badala ya kutegemea kuuza mazao bila kuyafanyia uchakataji.

Katika hatua nyingine, Waziri Kapinga amesema Serikali inatambua upatikanaji wa mitaji kuwa nguzo muhimu katika kukuza ujasiriamali na kuendeleza viwanda vidogo, hivyo inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya upatikanaji wa mikopo nafuu kupitia mifuko ya taifa inayolenga kuwawezesha wajasiriamali.

“Lengo la Serikali ni kuhakikisha huduma hizi zinawafikia wajasiriamali wengi zaidi, ili waweze kuanzisha na kuendeleza biashara zao, kuongeza uzalishaji na kutengeneza ajira,” amesisitiza.

Aidha, amezihimiza taasisi za fedha kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuwawezesha wajasiriamali kupata mitaji, huku akiwataka wafanyabiashara kuandaa mipango madhubuti ya biashara itakayowawezesha kutumia mikopo kwa tija na kuendeleza shughuli zao kwa uendelevu.

Ameeleza kuwa ushirikiano kati ya Serikali, SIDO, taasisi za fedha na sekta binafsi ni muhimu katika kujenga mazingira yatakayowezesha biashara ndogo kukua na kuwa viwanda imara vinavyochangia ajira na mapato ya wananchi.

Waziri Kapinga amewataka washiriki kuyatumia maonesho hayo kuanzisha mikataba ya kibiashara na mahusiano ya kudumu na wanunuzi badala ya kuishia kuonesha bidhaa pekee.

Pia amewahimiza wajasiriamali kutumia teknolojia za kidijitali kutangaza na kusambaza bidhaa zao ili kuwafikia wateja wengi zaidi, huku akiwataka Watanzania kuendelea kununua bidhaa zinazozalishwa nchini ili kuchochea ukuaji wa viwanda vya ndani na uchumi wa Taifa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Dkt. Francis Mlacha, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amesema Mkoa wa Shinyanga unaendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji kwa kutenga maeneo maalumu yenye ukubwa wa takribani hekta 5,477 katika halmashauri za mkoa huo, kwa lengo la kuvutia uwekezaji na kuchochea maendeleo ya viwanda na biashara.

Maonesho hayo ya kitaifa yanatoa fursa kwa wajasiriamali kutangaza bidhaa na huduma zao, kujifunza teknolojia mpya, kutafuta masoko na kujenga mahusiano ya kibiashara.


Post a Comment

0 Comments