6/recent/ticker-posts

BENKI YA AZANIA TAWI LA SHINYANGA KUWAJENGEA UWEZO WASTAAFU KUHUSU USIMAMIZI WA FEDHA

Benki ya AZANIA, Tawi la Shinyanga, inatarajia kuendesha semina maalumu kwa wastaafu zaidi ya 300, ikiwa na lengo la kuwajengea uwezo kuhusu usimamizi na matumizi bora ya fedha, pamoja na kuwafahamisha huduma mbalimbali za kibenki zinazotolewa na benki hiyo.

Semina hiyo  ambayo itaanza saa 2:00 asubuhi, inatarajiwa kufanyika kesho Jumanne tarehe 17, Novemba 2026, katika Bwalo la Jeshi, Kambarage mjini Shinyanga, na itawakutanisha wastaafu kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Shinyanga.

Akizungumza kuhusu maandalizi ya semina hiyo, Afisa Mahusiano wa Benki ya AZANIA, Tawi la Shinyanga, Novatus Grevase, amesema washiriki watapata elimu kuhusu huduma za kibenki zinazotolewa na benki hiyo, hususan mikopo na namna bora ya kusimamia na kutumia fedha wanazopata.

Afisa Mahusiano wa Benki ya AZANIA, Tawi la Shinyanga, Novatus Grevase

Amesema elimu hiyo inalenga kuwasaidia wastaafu kufanya maamuzi sahihi ya kifedha, kutumia mikopo kwa shughuli zenye tija na kuhakikisha fedha wanazokopa zinachangia kuboresha maisha yao, badala ya kuwa mzigo wa kifedha.

Aidha, amesema semina hiyo itashirikisha taasisi mbalimbali ambazo ni wanahisa wa Benki hiyo, ambao ni pamoja na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa Sekta binafsi (NSSF) na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Wadau hao kwa pamoja watatoa elimu juu ya huduma mbalimbali wanazozitoa ,hususan zinazowalenga wastaafu.

Benki ya AZANIA ambayo inatoa huduma za kifedha katika maeneo mbalimbali nchini, imeendelea kuweka mkazo katika suala la kuwainua wananchi kiuchumi, kwa kutoa mikopo maalumu yenye riba nafuu na masharti yanayozingatia mahitaji ya makundi mbalimbali ya kijamii.

Makundi hayo ni pamoja na wastaafu, wanawake, wakulima, wafanyabiashara, vikundi vya wajasiriamali, watumishi wa sekta binafsi na watu binafsi.

Post a Comment

0 Comments