6/recent/ticker-posts

MGODI WA NORTH MARA KINARA TUZO ZA TRA KWA UZINGATIAJI KANUNI ZA KODI NCHINI


Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Yusuph Mwenda (kulia) akikabidhi tuzo kwa Meneja uhusiano na Mawasiliano wa Barrick Tanzania Georgia Mutagahywa wakati wa hafla ya tuzo za mlipa kodi bora 2025 ambapo Mgodi wa Barrick North Mara uliibuka kidedea katika uzingatiaji kanuni za kodi nchini
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Yusuph Mwenda (kulia) akikabidhi tuzo kwa Meneja uhusiano na Mawasiliano wa Barrick Tanzania Georgia Mutagahywa wakati wa hafla ya tuzo za mlipa kodi bora 2025 ambapo Mgodi wa Barrick North Mara uliibuka kidedea katika uzingatiaji kanuni za kodi nchini
Mgodi wa dhahabu wa North Mara ambao uko chini ya Twiga Minerals Corporation umepata tuzo ya uzingatiaji kanuni za kodi nchini kitaifa na kwenye sekta ya madini katika kipindi cha mwaka wa 2023/24 katika hafla ya utoaji wa tuzo kwa walipa kodi iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliyofanyika jijini Dar es Salaam.


Kampuni ya Twiga ni ya ubia kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kampuni ya Barrick Gold Corporation. Inasimamia uendeshaji wa migodi ya dhhabu ya Bulyanhulu uliopo mkoani Shinyanga, North Mara uliopo Tarime mkoani Mara na Buzwagi (Pangea) uliopo mkoani Shinyanga ambao umefungwa na eneo lake kugeuzwa kuwa kongani ya biashara (Special Economic Zone).


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, alikuwa Mgeni Rasmi katika hafla hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa The Dome jijini Dar es Salaam.


Mheshimiwa Rais Samia aliipongeza TRA kwa kazi nzuri inayofanya katika ukusanyaji wa mapato. Rais alizidi kuipongeza taasisi hiyo kwa kupanua wigo wa kodi na pia kuwekeza katika teknolojia muhimu ambayo imechochea ufanisi wake kutokana na uwezo wake wa kuunganishwa na mifumo mingine ya serikali.


Katika kipindi cha mwaka 2024, Twiga Minerals Corporation ililipa kodi ya mapato kiasi cha dola milioni 92,Mwaka 2023 ililipa dola milioni 58 na kipindi cha mwaka cha 2022 ililipa dola milioni 112


Akiongea katika mkutano wa robo mwaka wa kueleza shughuli za utendaji wa kampuni uliofanyika katika mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu wiki, Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Barrick Gold Corporation,Dk. Mark Bristow, alisema kuwa Twiga imechangia zaidi ya dola bilioni 4.24 katika uchumi wa Tanzania kuanzia kipindi cha mwaka 2019. Kati ya hizo, dola bilioni 1.37 zililipwa kwa njia ya kodi na tozo mbalimbali za serikali.


Kuhusu uwezeshaji wa biashara za ndani, Dkt. Bristow alisema kuwa asilimia 83% ya manunuzi ya kampuni mwaka 2024, ambayo yalifikia dola za kimarekani milioni 573, yalifanywa hapa nchini. Kampuni imetumia dola kimarekani bilioni 2.3 kwa manunuzi ya ndani tangu mwaka 2019.

Post a Comment

0 Comments