6/recent/ticker-posts

VITA YA URAIS KATI YA LISSU NA MBOWE YAIPASUA CHADEMA

 

*Vita ya urais kati ya Lissu na Mbowe yaipasua CHADEMA

* Mgogoro mkubwa wa madaraka waibuka kuwania ugombea urais 2025

* Lissu akianika chama chake hadharani, asema CHADEMA imekithiri rushwa

* Ashutumu uongozi wa chama kumnyima pesa za maandamano na mikutano ya hadhara

Mei 3, 2024

Na Mwandishi Wetu _ Iringa


Vita kubwa ya madaraka kati ya Tundu Lissu na Freeman Mbowe imeibuka ndani ya CHADEMA na kukipasua chama hicho kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani.


Chimbuko la mgogoro huo wa maslahi ni nani ateuliwe na CHADEMA kuwania urais mwaka 2025 kati ya Lissu na Mbowe.


Mgogoro huo kati ya Mbowe na Lissu umekuwa ukifukuta chini kwa chini ndani ya chama kwa takribani miaka minne, kabla ya kuibuka rasmi hadharani.


Hii ni baada ya Lissu kutangaza jukwaani jana mkoani Iringa kuwa rushwa imekithiri kwenye uchaguzi wa ndani wa CHADEMA, ikiashiria kuwa yeye na Mbowe wanapambana kupanga safu zao za viongozi kwenye chama hicho nchi nzima ili wawasaidie kuupata ugombea urais.


"Kuna mtafaruku mkubwa sana wa uchaguzi ndani ya chama chetu," Lissu alisema jana mwenye mkutano wa hadhara Iringa.


"Kuna pesa nyingi ajabu kwenye uchaguzi huu (ndani ya CHADEMA)."


Lissu alilalamika kuwa amekuwa akiambiwa na uongozi wa chama chake kuwa hakuna pesa za kulipia mikutano yake ya hadhara, lakini anashangaa kuona kuna pesa za rushwa kwenye uchaguzi wa ndani.


Maandamano na mikutano ya Lissu mikoani yanaonekana kukosa mvuto na kupata watu wachache kulinganisha na mikutano ambayo imekuwa inafanywa na Mbowe.


Kitendo cha Lissu kulalamika hadharani kuhusu rushwa ndani ya chama na kunyimwa pesa za maandamano na mikutano ya hadhara, kimetafsiriwa na baadhi ya Wanachadema kama utovu wa nidhamu na kukidhalilisha chama.


Utaratibu wa CHADEMA ni kuwa kiongozi huyo alitakiwa kuwasilisha malalamiko yake kwenye vikao rasmi vya ndani vya chama, ikiwemo Kamati Kuu, siyo jukwaani.


 *MAFAHALI WAWILI, ZIZI MOJA* 


Kambi ya Lissu inadai kuwa Lissu ananyimwa pesa za mikutano na chama kwa makusudi na nguvu zote zinapelekwa kwa Mbowe ili ionekane kuwa Mbowe anakubalika zaidi na wananchi kwani mikutano yake hujaza watu zaidi ya Lissu.


Mbowe na Lissu wote wamewahi kugombea urais mara moja na kushindwa na mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).


Taarifa kutoka ndani ya CHADEMA zinasema kuwa Mbowe na Lissu wote wanataka kugombea urais kupitia chama hicho mwaka 2025 na hiyo ndiyo sababu kuu ya mtafaruku ndani ya chama hicho.


Hali hii imesababisha CHADEMA kumeguka katikati kwenye kambi mbili.


Kambi moja ina viongozi na wanachama ambao wanamuunga mkono Mwenyekiti Mbowe na wanamuona yeye ndiyo mtu sahihi wa kuivusha CHADEMA kama mgombea urais mwakani.


Kambi ya pili iko na Lissu na inamtaka Makamu Mwenyekiti huyo wa CHADEMA awe mgombea urais.


Lissu anaonekana kumuunga mkono Mwenyekiti wa CHADEMA wa Kanda ya Nyasa, Peter Msigwa, dhidi ya Joseph Mbilinyi 'Sugu' ambaye anawania nafasi hiyo kwenye uchaguzi wa ndani wa chama hicho.


Licha ya uongozi wa CHADEMA kumkataza Lissu asifanye mkutano Iringa, asubiri hadi uchaguzi wa ndani upite, Lissu alikaidi maagizo ya chama na kufanya mkutano na kutangaza hadharani kuwa kuna mtafaruku mkubwa na rushwa ndani ya chama.


Lissu aliwataka wanachama wa CHADEMA nchi nzima kutochagua viongozi wanaotumia pesa kwenye uchaguzi, ikiwa anaonekana kurusha tuhuma kwa Sugu ambaye anasemekana kuwa karibu na Mbowe.


Wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini wanasema kuwa vita ya Mbowe na Lissu inatarajiwa kupamba moto zaidi siku zijazo, kwani mafahali hao wawili hawawezi kuishi kwenye zizi moja.


Mgogoro wa madaraka na tuhuma za rushwa ndani ya CHADEMA zinaibua maswali kuwa chama hiki kinachojipambanua kama mbadala wa CCM, iwapo kweli kiko tayari kuongoza nchi.

Post a Comment

0 Comments