Na Amos John Shinyanga
Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Shinyanga, Askofu Johnsoni Chinyong'ole, amemsimika Mchungaji Canon Joan Ndabakubije (Mama Ndaba) kuwa Area Dean na Archdeacon wa Dinari ya Kitangili, Manispaa ya Shinyanga Magharibi.
Hii ni mara ya kwanza kwa mwanamke kuchaguliwa kushika cheo hiki katika historia ya kanisa la Anglikana katika eneo hilo.
Zoezi la kumsimika Mchungaji Canon Joan Ndabakubije limefanyika Novemba 1, 2024, katika ibada maalum iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Andrea Kitangili, Manispaa ya Shinyanga.
Ibada hiyo imehusisha pia uzinduzi wa Dinari ya Kitangili, Manispaa ya Shinyanga Magharibi.
Katika ibada hiyo, Askofu Chinyong'ole ametoa pongezi kwa Mchungaji Joan Ndabakubije, akimpongeza kwa mafanikio yake ya kiroho na huduma yake ya uongozi katika kanisa.
Askofu Chinyong'ole amesema uteuzi wa Mchungaji Joan Ndabakubije ni matokeo ya utendaji wake bora katika kuhubiri neno la Mungu na kueneza injili, huku akitaja mfano wake wa kuanzisha Kanisa la Mtakatifu Michael katika Kata ya Kizumbi kama ishara ya utumishi wa kujitolea.
Aidha, Askofu Chinyong'ole amewataka wachungaji na viongozi wa makanisa mengine kuiga mfano wa Mchungaji Canon Joan Ndabakubije katika kujitolea na kujenga jamii kwa kupitia huduma ya kiroho.
Kwa upande wake, Mchungaji Canon Joan Ndabakubije ametoa neno la shukrani kwa waumini na uongozi wa Dayosisi ya Shinyanga kwa kumteua kushika cheo hicho cha heshima.
Ameahidi kuendelea na kazi ya Mungu kwa moyo wake wote, huku akiahidi kutoa ushirikiano wa karibu kwa Askofu Chinyong'ole na wachungaji wengine wa Dayosisi ya Shinyanga katika kueneza neno la Mungu na kufanikisha huduma za kanisa.
Mchungaji Canon Joan Ndabakubije, ambaye pia anajulikana kama Mama Ndaba, ni kiongozi mwenye uzoefu na historia ya kujitolea katika huduma ya kiroho, na uteuzi huu unaonesha mafanikio yake na mchango wake mkubwa katika kanisa la Anglikana na jamii ya Shinyanga kwa ujumla.
0 Comments