6/recent/ticker-posts

USHIRIKIANO WA TAIFA GAS NA WASHIRIKA WAKE KUTOA ELIMU YA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA NA MATUMIZI YA NISHATI SAFI NI UKOMBOZI KWA WANAWAKE

  


Washiriki katika hafla hiyo wakifurahi baada ya kupatiwa khanga na mitungi ya gesi katika hafla hiyo
Mmoja wa washiriki akizawadiwa khanga yenye ujumbe wa kupinga ukatili wa kijinsia kutoka kwa Meneja wa Mahusiano ya Jamii na Mazingira wa mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Bw Agapiti Paul

***
-Wanawake wafurahia matumizi ya khanga kufikisha ujumbe

Jamii ya watanzania na wadau mbalimbali wameshauriwa kutumia maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano na njia nyinginezo za mawasiliano kama ambavyo vazi la khanga limetumika mwaka huu kufikisha ujumbe dhidi ya ukatii wa kijinsia (GBV) hapa nchini.

Akizungumza na wanawake wa kada mbalimbali mama lishe, walimu na wajasiriamali katika kilele cha siku 16 za kupiga ukatili wa kijinsia jana kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Afisa Tarafa wa Dakama, Tumshukuru Mudui, amesema kuwa siku 16 za harakati dhidi ya ukatili wa kijinsia zilizoambatana na mafunzo kwa wanawake ni hatua muhimu kuelekea jamii iliyo huru dhidi ya mateso ya wanawake na watoto.

"Ningependa kuchukua fursa hii kuishukuru Taifa Gas, Barrick, na washirika wengine kwa kushiriki na tukio hili la kipekee na la kibunifu lililolenga kuhamasisha mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia na kuelimisha jamii matumizi ya nishati safi (gesi) kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira hapa nchini," ameeleza.
Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Kahama ambaye ni Afisa Tarafa wa Dakama, Tumshukuru Mudui akiongea katika hafla hiyo.

Amesisitiza umuhimu wa ushiriki wa wanawake katika mafunzo na kusaidia kusambaza taarifa na elimu kuhusu ukatili huo katika shule za msingi na sekondari na kuunda mazingira bora kwa watoto wa shule kuelewa tatizo hili kutoka ngazi ya chini, kata, wilaya, mkoa hadi taifa.

Amelipongeza pia Jeshi la Polisi la Tanzania kwa kuanzisha dawati la jinsia kushughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia, huku wakishirikiana na washirika mbalimbali na taasisi nyingine katika kuendeleza mapambano hayo.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Barrick Bulyanhulu, Bw Victor Lule, amesema kwamba ni muhimu jamii kutumia kila njia ikiwemo kutumia kikamilifu maendeleo ya sayansi na teknolojia kama njia bora ya kushughulikia ukatili wa kijinsia kwenye ngazi zote kuanzia taifa, kikanda na kimataifa.
Meneja Mkuu wa Barrick Bulyanhulu, Bw Victor Lule akiongea

Bw. Lule ameongeza kuwa vitendo vya ukatili wa kijinsia ina athari mbaya kwa jamii, si tu kijamii na kiuchumi, bali pia kiafya na kimazingira kutoka kwa kaya hadi ngazi ya taifa.

Meneja wa Mahusiano ya Jamii na Mazingira wa mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Bw Agapiti Paul, amesema kuwa mafunzo ya siku 16 kwa wanawake wanaozunguka migodi yalikwenda vizuri na wanawake wamepata uelewa huu tatizo hilo na mwamko ni mkubwa na jinsi ya kuzishughulikia.

Meneja wa Mauzo wa Taifa Gas kanda ya Victoria, Bw Joshua Julius amesema wameamua kushiriki katika siku 16 za harakati dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa kutoan elimu ya nishati safi na majiko ya gesi kwa wanawake ambao ni wahanga wakubwa wa vitendo hivi katika juhudi za kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama na kuunga mkono jitihada za Dkt.  Samia Suluhu Hassan.
Meneja wa Mauzo wa Taifa Gas kanda ya Victoria, Bw Joshua Julius akiongea katika hafla hiyo.

Maria Sokoni (34), mwalimu kutoka Shule ya Sekondari ya Kakola ni miongoni mwa wanufaika wa mafunzo ya ukatili wa kijinsia, amesema anajua kuwa ukatili huo hauleti madhara ya kimwili tu, bali pia mateso ya kisaikolojia ambayo yanazuia wanawake kufikia malengo yao ya kijamii na kiuchumi.

Mnufaika mwingine wa mafunzo hayo ya ukatili wa kijinsia ambaye ni mama lishe amesema mafunzo kuhusu ukatili huo yalimsaidia kujua haki zake dhidi ya vitendo vya kikatili kama ubakaji na kupigwa.

Joyce Felix (28), ambaye mhitimu wa cheti cha masuala ya afya, amesema kuwa mafunzo hayo ni daraja kwa wanawake jinsi ya kujikomboa kutoka kwenye janga la ukatili wa kijinsia.

Barrick kwa kushirikiana na wadau wengi ambao ni Jeshi la Polisi la Tanzania kupitia dawati la jinsia, halmashauri za wilaya, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) kama Voluntary Service Overseas (VSO), Life Changing Foundation (LCF), Jadra, Hope for the Girls and Women (HGWT), kampuni ya sheria maarufu ya Bowmans, na kampuni maarufu ya uzalishaji na usambazaji wa gesi, Taifa Gas, walitumia siku 16 za ukatili wa kijinsia kutoa mafunzo ya kupinga ukatili wa kijinsia,matumizi ya nishati safi ,kugawa gesi na khanga zenye ujumbe katika juhudi za kuendeleza mapambano hayo.
Washiriki katika hafla hiyo wakifurahi baada ya kupatiwa khanga na mitungi ya gesi katika hafla hiyo
Washiriki wakifuatilia matukio mbalimbali wakati huohuo wametinga khanga zenye ujumbe wa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia
Washiriki wakifuatilia matukio mbalimbali wakati huohuo wamevaa khanga zenye ujumbe wa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia

Post a Comment

0 Comments