6/recent/ticker-posts

CHANGAMOTO ZA MAJI, UMEME, ARDHI NA MIUNDOMBINU ZAWASILISHWA KWA DC MTATIRO

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Wakili Julius Mtatiro akizungumza kwenye mkutano wake wa hadhara  Januari 14, 2025.


Na Mapuli Kitina Misalaba


Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, ameanza ziara ya kutembelea kila kijiji katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kwa lengo la kusikiliza changamoto na kero za wananchi ambapo Januari 14, 2025 DC Mtatiro ametembelea vijiji vitatu vya Kata ya Usanda, Tarafa ya Samuye, ambavyo ni Shabuluba, Ngaganulwa, na Nzagaluba.

Katika hotuba yake, Mtatiro amesisitiza umuhimu wa upandaji miti kama njia ya kuhakikisha upatikanaji wa mvua za kutosha na kupunguza madhara ya mazingira. "Mvua za uhakika zinapatikana ikiwa tumepanda miti ya kutosha maeneo mengi hapa yako wazi, hakuna miti madhara ya kutokuwa na miti ni makubwa, hatuwezi kupata mvua za kutosha Shinyanga kama wananchi hawatashiriki kwenye kampeni ya upandaji wa miti," amesema DC Mtatiro.

Ameongeza kuwa timu ya Wilaya itafika kwenye kila kijiji na kata ili kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika kampeni hiyo huku akielezea  juu ya hatari ya upepo kuharibu nyumba kutokana na ukosefu wa miti na kusisitiza umuhimu wa kuacha maeneo wazi yawe yamepandwa miti.

Katika eneo la usafi wa mazingira, Mtatiro amekumbusha wananchi kuhusu umuhimu wa kudumisha usafi ili kuepuka magonjwa kama kipindupindu. "Katika miaka iliyopita, kumekuwa na shida ya kipindupindu wilayani ni muhimu kuhakikisha tunatumia maji safi na sabuni mara kwa mara na kuwa na vyoo vya kisasa," ameeleza DC Mtatiro.

Mtatiro pia amegusia masuala ya elimu, akitoa onyo kali kwa wazazi wanaochelewesha watoto kwenda shule ambapo ameweka wazi kuwa mzazi yeyote atakayeshindwa kumpeleka mtoto wake shule ifikapo Ijumaa ya wiki hii atachukuliwa hatua kali, ikiwemo kulipa faini ya shilingi elfu 50 kabla ya kuruhusiwa kumpeleka mtoto shule. "Kama hujajiandaa vizuri, mpeleke mtoto shuleni na shati hilo hilo alilonalo. Sale utamalizana na mwalimu," ameongeza.

Ziara ya DC Mtatiro pia imebaini changamoto mbalimbali za wananchi, zikiwemo ukosefu wa maji safi, umeme, migogoro ya ardhi, na ubovu wa miundombinu ya barabara ambapo wananchi wameitaka serikali kuchukua hatua za haraka kuzitatua changamoto hizo ili kupunguza usumbufu unaowakumba  wakati huo huo DC Mtatiro ametoa maagizo kwa mamlaka husika kutembelea maeneo hayo na kuchukua hatua za haraka.

Pia, wananchi wamezungumzia changamoto ya ukosefu wa mikopo inayotolewa na Halmashauri ambapo DC  Mtatiro ameelekeza Halmashauri kuhakikisha wananchi wanaokidhi vigezo wanapatiwa mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na serikali.

Katika kijiji cha Ngaganulwa, Mtatiro amemuondoa Afisa Mtendaji wa kijiji, Sebastian Nkinga Tungu, baada ya kuripotiwa na wananchi kuwa analewa muda wote wa kazi ambapo amemwagiza Afisa Mtendaji wa Kata kumtafutia majukumu mengine nje ya kijiji hicho.

Mtatiro pia ametoa elimu kwa wazazi kuhusu umuhimu wa kuhakikisha watoto wanapata chakula shuleni ili kuboresha afya na ufaulu wao na kwamba ameonya kuwa mzazi atakayegoma kuchangia chakula kwa wanafunzi atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Ziara hiyo inaendelea na kwamba, ni sehemu ya juhudi za DC Mtatiro kusogeza huduma kwa wananchi na kushughulikia changamoto zinazowakabili katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Wakili Julius Mtatiro akizungumza kwenye mkutano wake wa hadhara katika kijiji cha Shabuluba Januari 14, 2025.

Post a Comment

0 Comments