Dar es Salaam, Januari 09, 2025.
Serikali ya Awamu ya Sita, kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), ilifanya mapinduzi makubwa katika kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya kwa mwaka 2024. Mafanikio haya yamedhihirishwa na ukamataji wa kiasi kikubwa cha dawa za kulevya na udhibiti wa mianya ya uingizwaji wa dawa hizo nchini. Pamoja na ukamataji wa dawa hizo, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ilijikita katika kutoa elimu juu ya madhara ya dawa za kulevya, kuimarisha huduma za matibabu ya waraibu kwa kuongeza vituo vya huduma za tiba na utengamao na kuimarisha ushirikiano na wadau ndani na nje ya nchi.
Kwa mwaka 2024, jumla ya kilogramu 2,327,983.66 za dawa za kulevya zilikamatwa. Hiki ni kiasi kikubwa cha dawa za kulevya kuwahi kukamatwa nchini na endapo kiasi hiki kingefanikiwa kusambazwa kingeleta athari kubwa na kurudisha nyuma ustawi wa Taifa letu.
Aidha, bangi ni dawa ya kulevya iliyokamatwa kwa wingi zaidi mwaka 2024 ikifuatiwa na methamphetamine, heroin na dawa tiba yenye asili ya kulevya aina ya fentanyl. Aidha, kwa mara ya kwanza dawa mpya ya kulevya aina ya 3-4 methylene-Dioxy-Pyrovalerone (MDVP) ilikamatwa nchini. Ufanisi huu umetokana na operesheni zilizofanyika katika maeneo mbalimbali ndani ya nchi yetu ikiwemo eneo la Bahari ya Hindi ambapo dawa za kulevya zimekuwa zikiingizwa kwa kiasi kikubwa nchini kupitia majahazi.
Katika operesheni zilizofanyika mwishoni mwa mwaka 2024, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola zilikamatwa kilogramu 673.2 za methamphetamine na heroin. Kati ya dawa hizo, kilogramu 448.3 zilizowahusisha raia nane (8) wa Pakistani zilikamatwa Bahari ya Hindi zikiwa zimefichwa ndani ya jahazi lililosajiliwa nchini Pakistani kwa namba B.F.D 16548. Aidha, kilogramu 224.9 zilikamatwa kwenye fukwe za Bahari ya Hindi mkoani Dar es Salaam.
Kwa upande mwingine, Serikali imeendelea kuweka mkazo katika kuhakikisha inaikinga jamii dhidi ya madhara yatokanayo na matumizi na biashara ya dawa za kulevya. Kwa mwaka 2024, takribani watu milioni 28 walipewa elimu kuhusu tatizo la dawa za kulevya kupitia nyanja mbalimbali za uelimishaji, zikiwemo vyombo vya habari, semina na warsha, matamasha, mikusanyiko mbalimbali, na matukio ya kitaifa.
Katika juhudi za kupanua huduma za tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya nchini, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, imeongeza vituo viwili vya matibabu (MAT Clinics) katika mikoa ya Pwani na Tanga, na hivyo kufanikisha kuwa na jumla ya vituo 18 vya MAT nchini. Vituo hivi vimesajili na vinawahudumia jumla ya waraibu 18,170. Vituo hivi vinatoa huduma za utengamao kwa waraibu wa dawa za kulevya aina ya afyuni kama vile heroin na baadhi ya dawa tiba zenye asili ya kulevya kama vile Tramadol na Pethidine.
Aidha, zimeongezeka nyumba sita (06) za upataji nafuu (Sober house) na hivyo, kufikia nyumba 62 ambapo jumla ya waraibu 17,230 walipata huduma za utengamao. Kadhalika, waraibu wengine wa dawa za kulevya na vilevi vingine zaidi ya laki tisa walihudumiwa katika vitengo vya afya ya akili vilivyopo kwenye hospitali za wilaya, mikoa na hospitali za rufaa za kanda.
Mafanikio haya yamefikiwa kutokana na uwekezaji wa Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwekeza kwenye afua za kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya na kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia ambayo yamekuwa chachu ya ushirikiano tunaoupata kutoka kwa wadau wetu wa ndani na nje ya nchi.
Tathmini ya upatikanaji na usambazaji wa dawa za kulevya inaonesha kuwa, dawa aina ya heroin zimepungua sana hapa nchini, hali ambayo imesababisha idadi kubwa ya waraibu kutumia dawa mbadala kama vile dawa tiba zenye asili ya kulevya na wengine kuhitaji matibabu baada ya kukosa dawa za kulevya mtaani. Vilevile, baadhi ya watu walianza kutengeneza dawa za kulevya zinazofanana na heroin kutokana na kuwepo kwa uhaba wa dawa hiyo na baadhi yao tumewakamata pia tunaendelea kufuatilia kwa karibu uwepo wa dawa mpya za kulevya (NPS).
Mwaka 2025, vipaumbele vya DCEA vitahusisha kuimarisha zaidi udhibiti wa dawa za kulevya kwa kuongeza ushirikiano wa kimataifa na matumizi ya teknolojia za kisasa kufuatilia mitandao ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya, utoaji wa elimu kwa umma ili kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na dawa za kulevya na kujiepusha na biashara na matumizi ya dawa za kulevya na kuendelea kuwasaidia waraibu wa dawa za kulevya kupitia programu za tiba na urekebishaji kupitia vituo vya tiba kwa waathirika vilivyopo nchini.
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inawashukuru kwa dhati wadau wote walioshiriki kwa namna mbalimbali katika kufanikisha mapambano dhidi ya tatizo la dawa za kulevya, vyombo vyote vya ulinzi na usalama, waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla kwani mchango wao umechangia kupata mafanikio makubwa.
Pia, Mamlaka inawaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za uhalifu wa dawa za kulevya kwa kupiga simu bure kupitia namba 119. Taarifa zinazotolewa zitapunguza usambazaji wa dawa za kulevya na kuikinga jamii isijiingize kwenye matumizi ya dawa hizo. Vita dhidi ya dawa za kulevya si jukumu la serikali pekee, bali ni jukumu la kila mtanzania mwenye mapenzi mema kwa Taifa hili. Tukishirikiana, tunaweza kulinda mustakabali wa Taifa letu dhidi ya janga la dawa za kulevya.
Kataa Dawa za Kulevya Timiza Malengo yako!
Imetolewa na,
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali
MAMLAKA YA KUDHIBITI NA KUPAMBANA NA DAWA ZA KULEVYA.
0 Comments