6/recent/ticker-posts

TAKUKURU Kahama Yatoa Onyo kwa Wagombea na Wananchi Dhidi ya Rushwa Katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa





Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani Kahama mkoani Shinyanga, Abdalah Urari, amewaonya wagombea na wananchi dhidi ya kushiriki vitendo vya rushwa wakati wa mchakato wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa, unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024, na Uchaguzi Mkuu wa Serikali Kuu mwaka 2025. Onyo hili limekuja baada ya TAKUKURU kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari na jamii kuhusu mwelekeo wa uchaguzi na athari za rushwa.


Ofisa wa TAKUKURU kutoka wilayani Kahama, Mlamuzi Pius Kuhanda, alisisitiza kuwa rushwa ni kosa la kimaadili na kiimani, na inapaswa kupigwa vita kwa nguvu zote. Kuhanda alieleza kwamba rushwa inaonekana kwa namna mbalimbali, ikiwa ni pamoja na wagombea kutoa rushwa kwa njia ya pesa, vitenge, sabuni, au tisheti kwa wananchi ili kupata kura. Viongozi na wananchi wanaoshiriki vitendo vya rushwa wanapaswa kujua kwamba ni kosa kisheria na kimaadili.


Kuhanda pia alieleza kwamba uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa ni muhimu katika kutengeneza mwelekeo wa uchaguzi ujao, kwani unasaidia kuibua viongozi bora watakaosaidia katika maendeleo ya jamii. Alihimiza jamii kubadilisha mtazamo na kuangalia wachukuliwaji rushwa kama wahalifu na sio mashujaa.


Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Kahama, Abdallah Urari, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya TAKUKURU, waandishi wa habari, na jamii katika kuzuia rushwa. Aliongeza kuwa TAKUKURU imekuwa ikitoa elimu kuhusu rushwa kwa makundi mbalimbali ikiwemo Boda Boda, viongozi wa dini, na mashuleni, ili kuhakikisha jamii inapata ufahamu wa kutosha kuhusu madhara ya rushwa.


Aidha, Ofisa Mchunguzi wa TAKUKURU Wilaya ya Kahama, Happnes Bilakwate, alitoa wito kwa wananchi kufuatilia mitandao ya kijamii ya taasisi hiyo ili kupata taarifa muhimu kuhusu sheria na vitendo vya rushwa. Alisisitiza umuhimu wa waandishi wa habari katika kuhamasisha jamii kuhusu kupinga rushwa na kuwasaidia wananchi kuelewa haki zao. 


Takukuru inasema kuwa rushwa ni adui wa maendeleo na kwamba kila mmoja ana jukumu la kuhakikisha inatokomezwa nchini.










Post a Comment

0 Comments