Na MWANDISHI WETU,
Dar es Salaam. Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umetoa semina kwa waajiri wa sekta binafsi wanaohudumiwa na Ofisi ya NSSF Mkoa wa Ubungo, Dar es Salaam.
Semina hiyo ilifanyika mwishoni mwa wiki katika Ofisi za NSSF Ubungo ikiwa na lengo la kuwakumbusha waajiri majukumu yao yakiwemo kusajili wafanyakazi wao na kuwasilisha michango kwa wakati kwani hilo ni takwa la kisheria.
Katika semina hiyo mada mbalimbali zilitolewa ikiwa ni pamoja na matakwa ya Sheria ya Mfuko na Matumizi ya Mifumo ya Tehama iliyoboreshwa (Employer Portal). Vilevile, mada kutoka Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Ubungo ziliwasilishwa na Bi. Devotha Mihayo, ambaye ni Mkuu Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Ubungo.
Akifungua semina hiyo, Meneja wa NSSF Mkoa wa Ubungo, CPA. Joseph Fungo amewashukuru waajiri wa sekta binafsi kwa kushiriki semina hiyo yenye lengo la kutoa elimu ya hifadhi ya jamii kwa waajiri pamoja na kuwakumbusha waajiri kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria ikiwa ni pamoja kutoa taarifa za wafanyakazi wasiosajiliwa ili Mfuko uweze kuwasajili na kisha kuwasilisha michango kwa wakati
Aidha, CPA. Fungo alieleza kuwa suala la kutoa elimu kwa wanachama na waajiri wa sekta binafsi wa mkoa huo litaimarisha ushirikiano kwa waajiri na Mfuko na kuongeza mafanikio ya utoaji wa huduma bora kwa wanachama na wadau kwa ujumla.
Kwa upande wake, Bw. Geofrey Ngwembe, Afisa Sheria wa NSSF ametumia semina hiyo kuwakumbusha waajiri hao kutekeleza wajibu wao kisheria katika kuhakikisha michango ya wanachama inawasilishwa kwa wakati pamoja na kuwajengea uelewa kuhusu maswala mbalimbali yanayohusu sheria ya hifadhi ya jamii.
0 Comments