Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango
amesema kufunguliwa kwa matawi ya Benki karibu na wananchi kutasaidia
kuondokana na wakopeshaji binafsi maarufu kama kausha damu ambao licha ya
kutoza riba kubwa, wananyanyasa na kutweza utu kwa vitendo vya ukamataji mali
za wadaiwa.
Makamu wa Rais amesema hayo mara baada ya kuzindua Tawi la Benki ya
NMB Chanika na Tawi la Benki ya NMB Kinyerezi Jijini Dar es Salaam ambapo amesema
uzinduzi wa matawi hayo ya Benki utachangia maendeleo ya Taifa kwa kulipa kodi
mbalimbali na kutoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.
Hali
kadhalika, amesema tawi la Benki hiyo litawezesha kufanyika kwa usalama zaidi
wa miamala mbalimbali kama vile malipo ya bili za maji na umeme, ada za shule
na mauzo ya bidhaa mbalimbali.
Makamu wa Rais ametoa wito kwa Benki ya NMB
kuendelea kushiriki katika kutatua changamoto mbalimbali za kijamii ikiwemo
katika sekta ya Afya na Elimu. Amesema uwajibikaji kwa jamii ndio msingi imara
wa mahusiano bora na yenye tija kati ya benki na jamii.
Aidha ameongeza kwamba
kwa kuendelea kuongeza idadi ya mawakala kutasaidia katika kuzalisha ajira kwa
vijana ambao ndio wadau wakubwa huduma hizo.
Vilevile, Makamu wa Rais amesema
ni vema kuelekeza nguvu zaidi katika kukuza elimu na uelewa kuhusu masuala ya
fedha ambao umeonekana kuwa mdogo miongoni mwa wananchi.
Ametoa wito kwa Benki
ya NMB kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania na Umoja wa Mabenki kubuni
programu na mikakati zaidi ya kuongeza elimu kwa Watanzania, hususan kwa wale
waishio vijijini.
Amesema ni muhimu kuangalia namna bora ya kupunguza gharama
za huduma za kibenki za kidijiti ambazo baadhi zinaonekana kuwa kubwa na hivyo
kukinzana na lengo la Taifa kupunguza matumizi ya fedha taslimu ili kurahisisha
malipo, kuchochea matumizi na kuipunguzia Serikali gharama za kutengeneza
sarafu.

0 Comments