6/recent/ticker-posts

MIL.255 ZA TOLEWA NA MANISPAA YA SHINYANGA KWA VIKUNDI 19, DC MTATIRO AWATAKA WALIOKOPA KURUDISHA KWA WAKATI


Chanzo na - Malunde 1 blog

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Wakili Julius Mtatiro amewataka Wanavikundi ambao wamepokea Mikopo ya asilimia 10 ya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kuitumia mikopo hiyo kwenye Miradi waliyoiorodhesha wakati wanaomba mikopo huku akiwasihi wairejeshe mikopo hiyo kwa wakati kwani mikopo hii ni ya hiari lakini urejeshaji ni lazima.

DC Mtatiro ameyasema haya leo Aprili 2, 2025 kwenye Hafla ya utoaji mkopo kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu, hafla iliyofanyika kwenye Viwanja vya Soko Kuu la Manispaa ya Shinyanga ambapo pamoja na yote amempongeza Mkurugenzi Mtendaji Mwl. Alexius Kagunze, Katibu Tawala Wilaya na Meya wa Manispaa ya Shinyanga kwa ukusanyaji mzuri wa mapato ambayo yanasaidia katika uwezeshaji na utoaji wa mikopo hii ambayo inawanufaisha na kuwawezesha wananchi kiuchumi.

“Ninawasisitiza wanavikundi ambao mmepata mikopo hii mkaitumie kwenye miradi ambayo mliiorodhesha kipindi mnaomba mikopo na msijaribu kuitumia fedha ambazo mmepata kwenye miradi mingine ambayo hamkuiorodhesha kwani kufanya hivyo ni kinyume cha kanuni na taratibu, lakini pia ninawasihi muirejeshe mikopo hii kwa wakati kulingana na muda ambao umewekwa kwani kukopa ni hiari lakini kurejesha ni lazima”, amesema DC Mtatiro.

Aidha DC Mtatiro amewasihi wanavikundi ambao wamepata mikopo hii kuwatafuta Maafisa Maendeleo Kata, Halmashauri na Wilaya katika maeneo wanayoishi na kuwasiliana nao kwa ukaribu pindi wanapopata changamoto kwenye urejeshaji wa mikopo ili waweze kusaidiwa na kutafuta suluhu za changamoto ambazo huenda wakapitia badala ya kusubiri mpaka watafutwe pindi wanaposhindwa kurejesha.

Kwa upande Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Ndg. Peres Kamugisha akiwasilisha taarifa ya utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu amesema mpaka sasa wamekabidhi takribani Milioni 255 kwenye Vikundi 19 ambapo Vikundi 11 ni vya Wanawake, Vikundi 7 vya Vijana na Kikundi 1 cha Walemavu huku akiendelea kusisitiza kuwa mikopo hii ni endelevu na itaendelea kutolewa kwenye vikundi ambavyo vitakidhi kanuni na taratibu zilizopo.

Diwani wa kata ya Mjini Mhe. Gulamhafeez Mukadam akizungumza wakati wa gafla hiyo ya utoaji mikopo amewasihi vijana, kina mama na watu wenye ulemavu kuchangamkia fursa ya mikopo hiyo inayotolewa na manispaa ambayo haina lipa na kuepukana na mikopo ya Kausha damu inayotolewa mtaani.

Aidha Wawakilishi wa Vikundi vilivyopata mikopo ya asilimia 10 kwa nyakati tofauti wameishukuru Serikali kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kwa kutoa mikopo hiyo ambayo inaenda kuwawezesha kiuchumi kupitia biashara mbalimbali wanazofanya lakini pia wameahidi kwenda kufanya kazi kwa bidii ili kuirejesha mikopo hiyo kwa wakati na wengine pia wanufaike.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Wakili Julius Mtatiro akizungumza wakati wa hafla hiyo ya utoaji wa mikopo.

Mstahiki Meya Manispaa ya Shinyanga Elias Masumbuko akizungumza wakati wa hafla hiyo ya utoaji wa mikopo.

Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Shinyanga Nyanjula Kiyenze akizungumza wakati wa hafla hiyo ya utoaji wa mikopo.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Ndg. Peres Kamugisha akiwasilisha taarifa ya utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu wakati wa hafla hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Wakili Julius Mtatiro akikabidhi hundi ya Shilingi Milioni 255.

Diwani wa kata ya Mjini Mhe. Gulamhafeez Mukadam akizungumza wakati wa gafla hiyo ya utoaji mikopo.

Pikipiki za mkopo zilizotolewa na manispaa ya Shinyanga kwa vijana.

Pikipiki za mkopo zilizotolewa na manispaa ya Shinyanga kwa vijana.



















Baadhi ya wananchi waliojitokeza kushuhudia hafla hiyo ya utoaji mikopo.








Penina Ezekiel mmoja ya waliopatiwa mikopo akitoa shukurani kwa kupatiwa mikopo hiyo.

Post a Comment

0 Comments